Aliyekuwa Mgombea Urais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameondoka nchini na kuelekea Ubelgiji.
Lissu ameondoka leo Novemba 10, 2020 ikiwa ni siku chache baada ya kuomba hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani nchini na kusema hakimbii mapambano bali anakwenda uwanja mwingine mpya wa kudai Haki.
Lissu aliyeomba hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani tangu Novemba 2, akidai kutishiwa maisha yake, amesema kuwa amesafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia itakayopitia Addis Ababa, kisha Vienna Austria na kituo cha mwisho kitakuwa Brussels, Ubeligiji.
Amesema anakwenda nchi hiyo kwa sababu tayari anayo ruhusa ya kuishi huko tangu alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Nakwenda Ubelgiji. Sio political asylum (hifadhi ya kisiasa), mimi nina ruhusa ya kukaa Ubelgiji tangu nilipokwenda kwa matibabu Januari 2018. Kwa hiyo sihitaji kuomba political asylum,” amesema Lissu.
Lissu alirejea Tanzania Julai 27, 2020 akitokea nchini Ubelgiji na kushiriki mchakato wa kugombea urais kupitia Chadema ambapo chama hicho kilimpitisha.
Katika uchaguzi huo Lissu alishika nafasi ya pili nyuma ya Rais John Magufuli.