Mahakama Kuu ya Tanzania imepanga kesho, Agosti 15, 2019 kuanza kusikiliza kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akipinga uamuzi wa kuvuliwa ubunge wa jimbo hilo.
Chombo hicho cha haki kimetoa hati ya wito wa kumtaka Lissu kufika mahakamani hapo, ili kesi yake ianze kutajwa. Lissu aliwasilisha maombi ya kufungua shauri dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Shauri hilo la maombi namba 18 ya mwaka 2019 limepangwa kusikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Sirillius Matupa.
Juni 28, 2019, Spika Ndugai alitangaza kuwa amewasilisha barua kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kumueleza kuwa jimbo la Singida Mashariki liko wazi na anaweza kuitisha uchaguzi.
Spika Ndugai alitaja Ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zinaelezea kuwa mbunge atapoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge endapo atakosa mikutano mitatu mfululizo ya Bunge bila ruhusa ya Spika.
Alisema kuwa Lissu hajawahi kuwasilisha maombi ya ruhusa au kutoa taarifa ya maendeleo ya afya yake, licha ya kuwa anamuona akizunguka bara la Ulaya na Marekani akizungumza na vyombo vya habari.
Hata hivyo, Lissu ambaye ni mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), bado yuko nchini Ubelgiji tangu alipoenda kutibiwa majeraha yaliyotokana na kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 nje ya nyumba yake jijini Dodoma.
Mwanasiasa huyo amekuwa akiripotiwa kuwa amepanga kurejea nchini Septemba 7 mwaka huu, ikiwa ni kumbukizi ya siku ya tukio la kushambuliwa kwa risasi.