Mgombea urais kwa tiketi Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema kuwa licha ya Tume ya Taifa ya uchaguzi imemsimamisha kufanya kampeni ,anaendelea na maandalizi ya mkutano wake wa kampeni utakaofanyika keshokutwa Jumapili Oktoba 4.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam, Lissu amesema kuwa adhabu ya kutofanya kampeni kwa siku saba ni batili kwa kuwa yeye kama mgombea hakupewa barua ya kosa na muda wa kujibu tuhuma.
“Uamuzi huu sio wa haki, haki inadai mtuhumiwa apewe tuhuma zake kabla ya hukumu, na haikubaliki kwa namna yoyote, sheria ya maadili tunalazimishwa kusaini wagombea hivyo basi barua ingekuja kwangu na si kwenye Chama,” amesema Lissu.
Lissu amesisitiza kuwa msimamo wake ni kuendelea na kampeni siku ya Jumapili isipokuwa kama kikao cha kamati kuu ya chama kikisema asubiri siku saba zimalizike.
“Mimi najiandaa kwa kampeni za jumapili isipokuwa kama maamuzi ya kamati kuu ya chama kesho yatasema nisubiri siku saba”.