Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ambaye aligombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2020, amesema kwa sasa haiwazi nafasi hiyo.
Mwanasiasa huyo aliyerejea nchini hivi karibuni akitokea Ubelgiji alipokaa tangu mwaka 2018, ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Mwananchi, alipokuwa akizungumzia taarifa za kudaiwa kuitaka nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
Lissu alisema kiu yake sasa ni Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio nafasi hizo zinazotajwa.
“Siwazi urais, ubunge wala uenyekiti Chadema, kipaumbele changu ni Katiba…Katiba…Katiba,” alisema Lissu katika mahojiano maalum na gazeti la Mwananchi, nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam.
Aidha, alifafanua kuwa watu ambao wanaeneza taarifa zinazodai anaitaka nafasi ya uenyekiti wa Chadema, wana nia ya kutengeneza mtafaruku ili kupoteza dira ya nia ya kudai Katiba mpya.
Alisisitiza kuwa yeye na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe wana uhusiano mzuri na kwamba hata nafasi ya kuwa makamu mwenyekiti aliipata bila kuiomba, bali alipendekezwa akiwa nje ya nchi.
Lissu alirejea nchini kufuatia mazungumzo ya maridhiano ya kisiasa yanayoendekea kati ya Chama Cha Mapinduzi na Chadema.
Moja kati ya matokeo ya mazungumzo hayo yanayoendelea ni pamoja na kuruhusiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa na kukubaliana kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya.