Beki wa pembeni wa Majogoo wa Jiji ‘Livepool’ Trent Alexander-Arnold amesema mambo sio shwari klabuni hapo baada ya kuvurunda msimu huu 2022/23.
Liverpool imepata ushindi mfululizo katika michezo mitano ya Ligi Kuu England baada ya kupoteza alama nyingi msimu huu na kurudisha mwelekeo wa timu.
Kwa sasa Liverpool ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fulham iliyoupata juma lililopita.
Liverpool inaisogelea Man United kwa tofauti ya pointi tano kwani usiku wa kuamkia jana ilipokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Brighton. Hata hivyo ya ina mechi moja mkononi.
Beki huyo wa kimataifa wa England alisisitiza licha ya kushinda michezo mitano mfululizo hawana raha kutokana na msimu mbovu huku Liverpool ikiwa katika hatari kutofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Tumeshinda mechi tano mfululizo, hilo ndilo muhimu kwa sasa. Timu ilionyesha ukakamavu kwa sababu haikuwa rahisi. Hii imetuonyesha taswira yetu kwenye ligi tuendelee kucheza kwa bidii kwenye mechi nyingine zilizobaki.
Hatukupenda kuwepo hapa tulipo, kila mtu amesikitika mashabiki, makocha na wachezaji kwa ujumla. Tulitaka tuwe katika mbio za kuwania ubingwa, hatupo sawa kwa sasa kila mtu amevurugwa,” alisema Trent
Wakati huo huo Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp ana matumaini Liverpool itafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kusogea hadi nafasi ya tano.
Timu hiyo itacheza dhidi ya Brentford na Aston Villa katika Uwanja wa Anfield kwenye mechi nne za ligi zilizobaki. Mechi nyingine ni dhidi ya Leicester City na Southampton zote zitachezwa ugenini.