Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kutowazuia wabunge wa Chama cha Mapinduzi CCM, kushirikiana katika masuala ya kijamii na wabunge wa upinzani.
Ameyasema hayo siku chache baada ya Rais Magufuli kukutana na wabunge wa CCM Ikulu, Chamwino Mjini Dodoma, ambapo alikaririwa na vyombo vya habari akiwaambia wabunge hao kitendo cha baadhi ya wabunge kutaka kwenda kumtembelea Lema Gerezani ni kufanya usaliti ndani ya chama hicho.
Lowassa ameyasema hayo wakati wa ziara ya viongozi wa Chadema katika mikoa ya Pwani na Dar es salaam, wilayani Mkuranga.
“Namuomba Rais aisahihishe kauli hiyo ya kuwataka wabunge wa CCM, kutoshirikiana na wale wa upinzani, hii ni nchi yetu sote,” amesema Lowassa.
Aidha, katika ziara hiyo, Lowassa ameongozana na Meya wa Ubungo, Jacob Boniface pamoja na Mbunge wa viti Maalum Segerea Anatropia Theonest.
Hata hivyo, akizungumzia muungano wa vyama vya upinzani, amesema kuwa UKAWA ni muhimu kuliko wanavyodhani na kuongeza kuwa muungano wa vyama vya siasa katika Karne hii ni muhimu sana na kikubwa ni kuzingatia umoja na mshikamano.