Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye amerejea Chama Cha Mapinduzi akiachana na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewatumia salamu viongozi na wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani.
Lowassa ambaye leo amepokewa kwa shangwe na nderemo katika jimbo la Monduli aliloliongoza kwa miaka 20, ametuma salamu akiwashukuru viongozi wa chama hicho pamoja na wanachama wengine.
“Kwa Chadema, nawashukuru viongozi na wanachama, sana. Naomba msiniwekee maneno mdomoni,” amesema Lowassa.
Mwanasiasa huyo mkongwe alizikumbuka kura milioni sita alizopata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, alipogombea urais kupitia Chadema.
“Kwenye uchaguzi nilipata kura zaidi ya milioni sita, sio haba naomba wote mlionipigia kura tumuunge mkono Rais Magufuli,” alieleza.
Aidha, Mbunge huyo wa Monduli alisisitiza kuwa amerudi nyumbani na kwamba hataki watu wamuulize amerudi kufanya nini.
Lowassa alihama CCM Julai, 2015 baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa chama hicho kukata jina lake katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombe urais. Alijiunga na Chadema na kugombea urais akiungwa mkono na vyama vingine vya upinzani vilivyounda Ukawa.
Alipata kura milioni sita na kuweka historia ya kuwa mgombea wa upinzani kuwahi kupata kura nyingi zaidi tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa nchini, 1992. Dkt. John Magufuli aliyekuwa mgombea kupitia CCM alishinda urais akipata kura milioni nane.