Saa chache baada ya Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kutangaza kuibwaga Chadema na kutimkia CCM, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyempigia debe mwaka 2015 amewatia moyo wafuasi wake wa jimbo hilo.
Lowassa ambaye alikuwa Mbunge wa Monduli kwa zaidi ya miaka 20 amesema kuwa amepata taarifa za Kalanga kuhamia CCM na kwamba hilo kwake sio jambo la ajabu kwani ni haki yake ya kikatiba.
Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amewataka wananchi wa Monduli kuwa watulivu na kuhakikisha kuwa hawauzimi moto uliowashwa mwaka 2015.
“Najua kwamba watu wa Monduli, mimi mwenyewe tumesikitishwa na habari hizi, lakini nawaomba msivunjike moyo. Uamuzi wake utupe nguvu zaidi ya kupambana kwa ajili ya democrasia na mabadiliko ya kweli,” Lowassa amekaririwa.
“Moto tuliouanzisha mwaka 2015 hauwezi kuzimwa na mbinu hizi. Wengi watamfuata Kalanga, lakini moto unaowaka kwenye mioyo ya watu utaendelea,” aliongeza.
Kauli ya Lowassa inaonesha kuibeba tena Monduli na kujiandaa kwa ajili ya mapambano mapya ya kumsimika mgombea mwingine wa Chadema. Jana, kulikuwa na taarifa kuwa huenda mtoto wa Lowassa, Freddy Lowassa akagombea nafasi hiyo kutokana na mashinikizo ya wengi.
Hata hivyo, Lowassa alikataa kuweka wazi msimamo wake kuhusu taarifa hizo akisema kuwa bado hajaongea naye na hajapata taarifa hizo, hivyo atazungumza baada ya kujua kinachoendelea kwa upande huo.
Jon Mrema, Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na uenezi wa Chadema, amesema kuwa uamuzi wa Kalanga ulimshangaza na kwamba ulimshangaza zaidi alipoamua kutangaza kujiuzulu usiku wa manani.