Uongozi wa klabu ya Young Africans umekamilisha zoezi la kumsainisha mkataba kocha Luc Eymael, ambaye aliwasili nchini juma lililopita kwa lengo la kurithi mikoba ya Mwinyi Zahera.
Eymael aliwasili nchini na moja kwa moja alielekea Zanzibar kushuhudia kikosi cha Young Africans ambacho kilishindwa kufurukuta mbele ya Mtibwa Sugar kwa kufungwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati, kwenye michuano ya Kombe La Mapinduzi inayofikia tamati leo jumatatu.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji alirejea Tanznaia bara, na mara kadhaa alihudhuria mazoezi ya kikosi chake, huku akisubiri taratibu za kukamilishwa kwa ajira yake ndani ya klabu hiyo kongwe.
Kabla ya kukamilishiwa taratibu hizo mapema hii leo, kocha Eymael ametimiziwa ombi lake la kutaka kufanya kazi na Riedoh Berdien kama kocha msaidizi na viungo.
Eymael amejiunga na Young Africans akichukua mikoba ya Mwinyi Zahera ambaye alitimuliwa ndani ya kikosi hicho kutokana na kuwa na matokeo mabovu ndani ya Young Africans, huku kocha mzawa Charles Mkwasa akikaimu kwa muda.
Kabla ya kukamilisha taratibu za kusiani mkataba wa mwaka mmoja na uongozi wa Young Africans, Mbelgiji huyo alianza kazi na kikosi chake kinachojiaanda kumenyana na Kagera Sugar, Jumatano mchezo wa ligi.
Kocha Aymael amejiunga na Young Africans baada ya kuzifundisha klabu za AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Missile ya Gabon, AFC Leopard ya Kenya, Rayon Sport ya Rwanda, JS Kairouan ya Tunisia, Al Nasr ya Dubai, Al Merreikh ya Sudan, Polokwane City, Free State Stars, Black Leopard za Afrika Kusini na Tala’ea El Gaish ya Misri