Lugha ya Kiswahili imependekezwa kuwa Lugha ya Nne katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mwenyekiti wa baraza la mawaziri la SADC, Prof. Palamagamba Kabudi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kuwa baraza hilo limependekeza Lugha ya Kiswahili ianze kutumika katika ngazi ya baraza la mawaziri na katika ngazi ya kikao cha wakuu wa nchi katika kutoa hotuba au katika ngazi mbalimbali za kuongea.
Aidha, Prof. Kabudi amesema kuwa baraza hilo pia limependekeza kuwa siku zijazo Lugha ya Kiswahili itumike katika kutafsiri nyaraka za umoja wa jumuiya ya SADC.
”Kwetu ni sisi Watanzania ni heshima kubwa, Kiswahili ambacho ndiyo Lugha ya ukombozi kama itakubaliwa na wakuu wa nchi kuwa itakuwa Lugha ya Nne,”amesema Prof. Kabudi
Hata hivyo, kuhusu vikao vya wakuu wa nchi, amesema kuwa vikao hivyo vitafunguliwa siku ya jumamosi asubuhi jijini Dar es salaam na kufungwa siku ya jumapili Alasiri.