Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameagiza kusimamishwa kazi kwa viongozi wa jeshi la polisi wilaya ya Geita, mkoani Geita kufuatia tukio la mahabusu kutoroka.
Akizungumza leo wilayani humo, Waziri Lugola amesema kuwa tukio hilo la kutoroka kwa mahabusu Mei 21 mwaka huu limelifedhehesha jeshi la polisi na kwamba viongozi hao wameshindwa kuwachukulia hatua askari waliokuwa wanawalinda mahabusu hao.
Mahabusu takribani themanini walitoroka walipokuwa wanapelekwa mahakamani kusikiliza kesi zao, lakini kwa mujibu wa Waziri Lugola, watoro wanne walikamatwa na kurejeshwa mahabusu.
“Naelekeza moja kwa moja Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili ahakikishe ndani ya siku mbili hizi OCD wa Wilaya hii ya Geita, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya na Mkuu wa Kituo cha Polisi wa Geita, wote hawa watatu wasimamishwe kazi wakae pembeni kabisa ili tuweze kuona humu ndani kuna nini,” alisema Lugola.
Waziri huyo alieleza kuwa ingawa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita imeunda tume ya kulichunguza tukio hilo, Wizara pia itatuma tume nyingine ya uchunguzi.
Alisema kuwa baada ya kufika mahabusu na kuwahoji wanne waliokamatwa tena kati ya 80 waliokuwa wametoroka, wamegundua kuna mambo yaliyojificha ambayo yanapaswa kuchunguzwa vizuri.
Waziri Lugola ameagiza askari 8 waliokuwa wanawalinda mahabusu hao wakamatwe na kuwekwa rumande wakati taratibu nyingine mahsusi zikichukuliwa.