Nahodha na kiungo wa timu ya taifa ya Croatia Luka Modric amesema timu yao ilikosa bahati ya kuibuka na ushindi dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa fainali, uliochezwa jana mjini Moscow, Urusi na kujikuta wakianguka kwa kuchapwa mabao manne kwa mawili.
Modric ambaye alitangazwa kuwa mchezaji bora wa fainali za kombe la dunia za 2018, amesema anaamini kikosi chao kilikua bora zaidi ya Ufaransa, lakini hali ya mchezo iliwakataa na kuruhusu kupoteza.
Kiungo huyo anaeitumikia klabu bingwa barani Ulaya (Real Madrid), amesisitiza kuwa tangu mwanzoni mwa fainali za kombe la dunia mwaka huu, kikosi chao kilionyesha soka safi hadi kufikia jana, na kila mmoja duniani alikikubali.
“Siku zote timu bora huwa haifanyi vizuri katika mchezo muhimu kama wa jana, lakini tunajivunia kwa mafanikio tuliyoyapata, tunaamini tumecheza vizuri lakini bahati haikua kwetu.
“Tunawapongeza Ufaransa kwa matokeo waliyoyapata, lakini hii haijatukatisha tamaa ya kuendeleza mapambano, tunaamini ipo siku bahati itakua kwetu, na sisi tutatawazwa kuwa mabingwa.” Amesema Modric
Kujivunia: “Nimejifunza mambo mengi katika kikosi chetu, hakuna mchezaji aliebweteka na mafanikio tuliyokua tunayapata kila tulipomaliza dakiak 90 ama 120 za mchezo, tulipambana kwa malengo hadi tunafika fainali.”
“Kupoteza kwa kufungwa mabao manne kwa mawili kwangu sio tatizo kubwa sana, kwani ninaamini na sisi tulionyesha kupambana, na wakati mwingine kila shabiki aliyekua anafuatilia mchezo alihisi huenda tungefanikiwa kuushangaza ulimwengu, lakini bado ninarudia kusema bahati haikua kwetu.”
Tuzo Ya Mchezaji bora Wa Mashindano: “Ninashukuru kwa mchango wangu kuonekana, ninaamini tuzo hii ilistahili kwangu, kutokana na juhudi na ushirikiano niliouonyesha kwa wenzangu, sina cha kusema zaidi ya kushukuru kila mmoja aliyefanikisha hili.
Mwamuzi: “Binafsi sikuona sababu ya penati waliopewa wenzetu, haikua makusudi kwa mchezjai wetu (Perisic) kuushika mpira katika eneo la hatari, lakini mwamuzi alifanya maamuzi na yameshawafaidisha wenzetu, tumekubali kupoteza.”
Kuelekea Fainali Za 2022: “Bado ni mapema mno kusema lolote, ninahitaji kupumzika na kujitathmini kama nitaweza kupambana hadi wakati huo, lakini tutarajie makubwa kutoka Croatia.”