Klabu ya Mbeya City imemtangaza rasmi Mathias Lule kutoka Uganda kuwa kocha mkuu wa kikosi cha klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21.
Mbeya City walimtangaza kocha huyo jana Jumatano (Desemba 02), baada ya kufanya upembuzi wa kina, kati ya makocha 14 wenye leseni A waliofikia hatua za mwisho za usaili.
Kati ya makocha hao 14, wanne walikua ni Watanzania na 10 ni kutoka nje ya Tanzania katika mataifa ya Rwanda, Uganda, Burundi, Ureno, Mexico na Italia, lakini Lule alikidhi vigezo vinavyotakiwa na klabu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Jiji la Mbeya.
Taarifa iliyotolewa na Mbeya City FC hiyo imesema Lule ambaye alikuwa ni kocha wa timu ya taifa ya Uganda *The Cranes* amepatikana kwa njia ya kupigiwa kura, akipata alama 41 za wajumbe wote wa bodi ya timu hiyo na anatarajiwa kutua nchini jana Jumatano (Desemba 02).
Mchakato wa kumsaka kocha mkuu wa Mbeya City, ulianza baada ya kocha mzawa Amri Said kusitishiwa mkataba wake mapema mwezi uliopita, kufuatia kushindwa kukidhi malengo ya klabu hiyo ambayo msimu uliopita iliponea chupuchupu kushuka daraja.
Kwa muda wa majuma kadhaa kikosi cha Mbeya City kilikua kikinolewa na kocha msaidizi Mathias Wandiba, ambaye amefanikiwa kuifikisha klabu hiyo kwenye nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.