Siku moja baada ya mabingwa wa soka Tanzania Bara kumtambulisha kiungo kutoka nchini Uganda Taddeo Lwanga, ufafanuzi umetolewa kuwa hatoweza kucheza katika kipindi hiki hadi dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Desemba 15.
Lwanga alitambulishwa rasmi jana mchana kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za Simba SC, na baadhi ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo waliamini huenda angeweza kuonekana uwanjani kwenye michezo ya Ligi Kuu inayofuata.
Kwa mujibu wa kanuni za usajili chini ya shirikisho la soka nchini TFF, klabu yoyote haitaruhusiwa kumtumia mchezaji aliesajiliwa baada ya dirisha kubwa kufungwa siku chache kabla ya kuanza kwa msimu mpya, lakini atakua na nafasi hiyo wakati wa dirisha dogo litakapofunguliwa.
Lwanga aliekabidhiwa jezi namba nne amesajiliwa Simba SC, baada ya kiungo kutoka nchini Brazil Gerson Fraga kusitishiwa mkataba wake, kufuatia kuwa majeruhi wa muda mrefu.
Lengo kubwa la Simba SC kumvuta kiungo huyo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo mkabaji ambapo atakuwa akishirikiana na mzawa Jonas Mkude, Mzamiru Yassini pamoja na Said Ndemla.