Kiungo mpya wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC Taddeo Lwanga jana Jumatatu (Desemba 07) alianza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake kwenye uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju jijini Dar es salaam.
Lwanga anaecheza nafasi ya kiungo mkabaji alitambulishwa rasmi na uongozi wa klabu ya Simba SC juma lililopita kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, akichukua nafasi ya kiungo Mbazil Gerison Fraga Vieira, alievunjiwa mkataba kufuatia kuwa majereha ya muda mrefu.
Lwanga alizungumza na Simba TV na kuesema kuwa, amekiona kikosi chake kipya kikiwa kazini jambo linalomfanya aongeze nguvu mazoezini, ili kupata namba kikosi cha kwanza.
“Nimekiona kikosi kwenye mchezo wetu dhidi ya Plateau United, kuna wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu hivyo nina amini kwamba nina kazi ya kufanya ili kuwa bora.”
“Kwa namna maisha hapa yalivyo ninafurahi kuwa hapa ninaamini kwamba tutashirikiana na wenzangu ili kupata kile ambacho tunakihitaji.”
Lwanga alikuwa jukwaaani wakati Simba ikitoshana nguvu ya bila kufungana na Plateau United kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Jumamosi (Desemba 5) Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kikosi cha Simba SC kinajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania, utakaochezwa kesho Jumatano (Desemba 09), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Lwanga ataanza kuitumikia Simba SC baada ya Dirisha Dogo la usajili kufunguliwa Desemba 15, lakini upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ataanza kutumika kwenye mchezo wa Raundi ya Pili ya michuano hiyo utakaoshuhudia Simba wakipambana dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe.