Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu ya Azam FC Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo, kuhusu hali ya Mshambuliaji Ayoub Lyanga, ambaye alilazimika kutolewa uwanjani dakika ya 81 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya awali dhidi ya Horseed ya Somalia, kufuatia kupata majeraha.
Zaka amesema Ayoub Lyanga ambaye alifunga bao la kusawazisha kwenye mchezo huo, hakupata majeraha makubwa sana, hivyo wanatarajiwa huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachopambana na Horseed kwenye mchezo wa mkondo wa pili utakaopigwa mwishoni mwa juma hili (Septemba 19) Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam.
“Lyanga hakupata majeraha makubwa ila baada ya mchezo ule kumalizika wachezaji walipewa muda wa mapumziko na wanatarajia kuanza mazoezi, kwa Lyanga kabla ya kuanza mazoezi atafanyiwa uchunguzi na madaktri ambao watatoa taarifa kwamba kama anaweza kuanza mazoezi au la,” amesema Zaka.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati amesema kuwa wanahitaji kupata ushindi kwenye mchezo wao wa marudio ili waweze kutinga hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Endapo Azam FC watapata matokeo mazuri kucheza mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Horseed, watakutana na Pyramid ya Misri.