Haruna Juma, Tanganyika – Katavi.

Halmashauri ya Wilaya Tanganyika Mkoa wa Katavi, imeanza maadhimisho ya siku ya Uhuru kwa kupanda miti 1000 katika kijiji cha Majalila zoezi lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Onesmo Buswelu akiambatana na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi – CCM, Wataalamu na wananchi.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, DC Buswelu amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kupitia wataalamu wake, kushirikiana na Wananchi wa Kijiji cha Majalila kutunza miti hiyo, kwa manufaa ya kizazi kijacho.

Aidha kutokana na miti hiyo kupandwa kando kando mwa Barabara kuu iendayo Kigoma, amemuagiza Katibu tawala wa wilaya ya hiyo kumwandikia barua meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Katavi ashirikiane na viongozi wa kijiji ili kuitunza miti hiyo kwa pamoja.

Kwa upande Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Hamad Mapendo amesema zoezi la upandaji miti katika wilaya ya Tanganyika ni endelevu na kwa sasa litaendelea ngazi ya kata na vijiji.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso alishauri Halmashauri itenge eneo maalumu kwa ajili ya zoezi la upandaji miti, wazo ambalo liliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya.

MSD yaongeza Majokofu ya kuhifadhia miili Manyara
Kagera waomba Meli ya Mizigo, RC Mwasa awapa uhakika