Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeitaka jamii kushirikiana katika malezi ya watoto, ili kuzuia tabia zisizozofaa zinazosabisha kuingia kwenye mkinzano wa Sheria na kujikuta wanawekwa mahabusu.
Hayo yamebainika wakati wa kikao cha Kamati hiyo na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum cha kupokea Taarifa ya utekelezaji wa Huduma za Mahabusu ya watoto mkoani Mbeya kilichofanyika Agosti 24, 2023 jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Riziki Said Lulida amesema suala la mmomonyoko wa maadili linachangia watoto kuharibika na kufikia hatua ya kufanya uhalifu hatimaye kuishia kwenye mahabusu za watoto huku akitaka juhudi katika kuliepusha Taifa na mmomonyoko wa maadili.
Naye mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuendesha mahabusu za watoto zinazosaidia watoto waliokinzana na sheria kuwa na mazingira rafiki ya kusikiliza mashauri yao na kuiomba jamii kila mmoja awajibike kwenye eneo lake kuhusu maadili na malezi ya watoto.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis amesema pamoja na Wizara kutoa elimu kwa jamii, wabunge na viongozi wote wanaombwa kuwa mabalozi wa malezi kwenye maeneo yao.