Maafisa wa Klabu ya Al Hilal ya Sudan wamekiri kuvutiwa na Uwezo wa Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasredine Mohamed Nabi, kwa kusema amefanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha WANANCHI.
Wakizungumza na Dar24 Media, maafisa hao waliotangulia jijini Dar es salaam kuweka mambo sawa kabla ya kuwasili kwa kikosi chao leo Alhamisi (Oktoba 06) majira ya saa kumi na mbili jioni, wamesema wanamfahamu Kocha Nabi baada ya kufanya kazi nchini Sudan akiwa na klabu ya Al-Mareikh.
Wamesema Kocha huyo ameonyesha uwezo mkubwa wa kuibadilisha Young Africans na kuwa moja ya klabu kubwa Afrika, ambayo ina uwezo wa kucheza na yoyote katika michuano ya Kimataifa.
“Tunamfahamu Nabi, alifanya kazi Sudan akiwa na Al-Mereikh, kwa kweli tangu alipokuja Tanzania kufanya kazi na Young Africans tumeona mabadiliko makubwa sana katika utendaji wake, ameifanya klabu hii kuwa na kikosi imara na tishio katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.”
“Binafsi nimekua naangalia sana michezo ya Ligi Kuu ya Tanzania hasa Young Africans inapocheza, nimeona mambo mengi ya kiufundi yaliyofanyiwa maboresho na kocha huyu, tofauti na alivyokuwa nyumbani Sudan akiitumikia Al -Mereikh.”
“Nilikua hapa wakati Young Africans ikicheza na Simba, niliona alivyofanya maajabu baada ya kutanguliwa kufungwa bao moja, kwa hakika ninakiri ni Kocha mzuri na mwenye mbinu nyingi sana.”
“Kwa hakika tumejipanga kukabilina naye, In Shaa Allah tunaamini mambo yatakuwa magumu katika mchezo wetu Jumamosi (Oktoba 08), ila tupo tayari kwa matokeo yoyote, iwe kufungwa, kushinda ama kutoka sare.” amesema Afisa wa Al Hilal
Nasredine Nabi akiajiriwa Young Africans April 2021, siku chache baada ya kufukuzwa Al-Mereikh, kufuatia matokeo mabaya kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.