Wazirio Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza makatibu tawala wa wilaya zote Tanzania Bara watekeleze majukumu kwa kuzingatia utawala bora, miiko na maadili ya viongozi wa umma.

Majaliwa ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akifungua semina elekezi kwa makatibu tawala wa wilaya.

“Kila mmoja akazingatie utumishi wa umma unaoongozwa kwa misingi ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya serikali. Misingi hiyo, ndio chachu ya ujenzi wa taswira nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita,” amesema Majaliwa.

“Kasimamieni kila sarafu na mhakikishe mnapata taarifa ya fedha zote zinazoingia katika halmashauri na mhakikishe miradi inatekelezwa kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha zinazotolewa”.

Aidha ameagiza wasome kwa makini na kuelewa sheria ya Tawala za Mikoa namba 19 ya mwaka 1997 ili kujenga uelewa kuhusu majukumu yao ya msingi na majukumu ya Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya.

“Kifungu cha 16 (1) kimetamka uwepo wa nafasi ya katibu tawala kwa kuteuliwa au kupangiwa lakini pia kifungu cha 16 (2) kimeweka bayana jukumu lako la kuwa wewe ndio mshauri mkuu wa mkuu wa wilaya katika kutekeleza wajibu wake na wako unaohusu serikali kuu na serikali za mitaa,” alisema.

Majaliwa amewataka wawe kiungo na kutengeneza mazingira wezeshi ya mahusiano kati yao, ofisi ya mkuu wa wilaya, ofisi ya mkuu wa mkoa, watumishi wa serikali kuu na watumishi waliopo katika mamlaka ya serikali za mtaa na wasimamie mwenendo wa vyama vya siasa na wadau wa maendeleo katika wilaya.

Aidha, aliwaagiza wazingatie utumishi wa umma unaoongozwa na misingi ya sheria, kanuni na taratibu na miongozo yakiwemo mawasiliano bora na mamlaka za juu.

EWURA yawaonya wafanyabiashara bei ya petrol, dizeli ikishuka
Usajili 2023/24: Dodoma Jiji nao wamo