Klabu za Ligi Kuu ya England, EPL, leo Jumatatu (Desemba 20) zitakutana kujadili nini cha kufanya, kutokana na janga la virusi vya Corona kuwaathiri wachezaji wengi.
Mameneja na manahodha pia watafanya mikutano yao.
Mejena wa Aston Villa, Steven Gerrard, amesema kuwa ana matumaini mkutano huo utaweka “mambo wazi” kuhusiana na “hofu kubwa zilizoko na maswali ambayo hayajajibiwa.”
Mtendaji Mkuu wa Ligi kuu England, Richard Masters ameziandikia klabu akitaka wachezaji wote wachanjwe na kusisitiza umuhimu wa kumalizika kwa msimu huu wa ligi kwa muda uliopangwa.
Naye Meneja wa Brentford, Thomas Frank, alikuwa wa kwanza kutoa wito wa kusitishwa kwa mechi zote hadi Desemba 26, mwaka huu ili kuwezesha kupangwa kwa mpango mpya.
Baadhi wanahisi mapumziko yanapaswa kuwa marefu zaidi, lakini wengine kama kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp haamini hilo linapaswa kufanyika.
Taarifa ya ligi hiyo ilisema Alhamisi kwamba, inalengo la kuendelea kucheza mechi ili mradi ni salama kufanya hivyo.