Rais wa Kenya, William Ruto amesissitiza kuwa hatorusu uchochezi wa ghasia katika nchi hiyo huku kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga akiwataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kushiriki maandamano ya nchi nzima leo Marchi 20, 2023.
Machi 19, 2023, Odinga alidai kuwa, “Tangu Ruto aapishwe miezi sita iliyopita ameendelea kuendesha nchi kwa dharau nyingi, Wakenya wengi hawawezi kustahimili gharama ya maisha na watu wengi wanakufa kwa sababu ya ukosefu wa chakula.”
Hata hivyo, Rais Ruto amesema kuwa hatamruhusu kiongozi huyo wa upinzani kuchochea ghasia nchini Kenya pia ameahidi kuwalinda waandamanaji wote na wale ambao hawatashiriki maandamano hayo.
“Raila Odinga hana sababu ya kutisha nchi kwa ghasia, maandamano na fujo, maafisa wa polisi watafanya kazi kwa mujibu wa sheria, watahakikisha haki za kila mtu zinalindwa (wakati wa maandamano ya Jumatatu),” amesema Ruto.
Naye, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amewahakikishia Wakenya kwamba polisi watalinda haki za raia wote, iwe watajiunga na maandamano au kuendelea na shughuli zao za kila siku.
“Mtu yeyote atakayechochea machafuko ya umma au kuvunja amani katika sehemu yoyote ya Jamhuri ya Kenya Jumatatu, Machi 20, atachukuliwa hatua za kisheria,” amesema.
Hata hivyo, maandamano hayo tayari yamezua wasiwasi miongoni mwa wamiliki wa biashara katika mji mkuu Nairobi, huku wengi wakitarajiwa kufunga maduka yao na hali ya wasiwasi ikiongezeka.
Maandamano ya wakati mmoja ya upinzani, yanapangwa kufanyika hii leo Machi 20, 2023 katika nchi sita za Afrika, ikiwa ni pamoja na Kenya, Nigeria, Senegal, Gambia, Tunisia, na Afrika Kusini, ingawa kwa malengo tofauti.