Serikali nchini Burundi imetangaza dharura ya kitaifa ya afya kutokana na mlipuko wa virusi vya polio Type 2 baada ya wagonjwa wanane kuthibitishwa, ikiwa ni mara ya kwanza kugundulika kwa virusi hivyo baada ya zaidi ya miongo mitatu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), iliyotolewa mjini Bunjumbura na Brazzaville,  virusi hivyo vimethibitishwa kwa mtoto wa kiume wa umri wa miaka minne katika wilaya ya Isale Magharibi mwa Burundi ambaye hajawwahi kupewa chanjo ya polio na pia kwa watoto wengine wawili waliokutana na mvulana huyo.

Akizungumzia mlipuko huo, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema “ Kubainika kusambaa kwa vitusi hivyo vya polio Burundi kunadhihirisha ufanisi ya mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa.”

Amesema, WHO inaunga mkono juhudi za kitaifa za kuongeza chanjo ya polio ili kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayekabiliwa hatari ya kupooza inayotokana na athari za polio.

Serikali ya Burundi, imepanga kutekeleza kampeni ya chanjo ya kukabiliana na polio katika wiki zijazo, inayolenga kuwalinda watoto wote wanaostahiki wenye umri wa miaka 0 hadi 7 dhidi ya virusi hivyo.

Mamlaka za afya, kwa msaada kutoka kwa WHO na washirika wa kimataifa wa mradi wa kutokomeza polio (GPEI), pia wameanza uchunguzi zaidi wa magonjwa, ikiwa ni pamoja na tathmini za hatari ili kubaini ukubwa wa mlipuko huo.

Polio Type 2 ni virusi inapatikana zaidi barani Afrika ambapo kumekuwa na wagonjwa 400 walioripotiwa katika nchi 14 kwa mwaka 2022.

Maandamano Kenya: Odinga auma na kupuliza
Wataalamu kuchunguza ugonjwa usiojulikana Kagera