Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Tumaini Nagu amesema Serikali imepeleka timu ya watalaamu wa afya katika Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuchunguza ugonjwa usiojulikana ambao umesababisha vifo vya watu wasiopungua watano.

Nagu ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa uchunguzi huo unafuatia uwepo wa Ebola nchini Uganda, ambao uliendelea kwa miezi minne na kusababisha vifo vya watu 55 kabla ya serikali kutangaza Januari kuuangamiza mlipuko huo.

Aidha Dkt. Nagu amesema vijiji walikotoka wagonjwa hao vimewekwa katika uangalizi maalumu na tahadhari mbalimbali zimetolewa kwa jamii ikiwemo kujiepusha kugusana mikono na kutowagusa watu wenye dalili za ugonjwa huo bila tahadhari.

Ugonjwa huo, ambao dalili zake zinashabihiana na dalili za ugonjwa wa Ebola ambao hivi karibuni uliripotiwa nchini Uganda, umesababisha taharuki kubwa kwa jamii nchini Tanzania hususan katika mkoa wa Kagera na maeneo yake ya jirani.

Waliopoteza maisha, ni pamoja na mtumishi mmoja wa zahanati ya Maruku mkoani Kagera ambaye anatajwa kuwa ndiye aliyemhudumia mgonjwa wa kwanza aliyefikishwa katika kituo hicho cha matibabu.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ilieleza kuwa, ugonjwa huo uligundulika katika jumla ya watu saba waliokuwa na dalili za homa, kutapika, kutokwa na damu katika sehemu tofauti za mwili na figo kushindwa kufanya kazi.

Serikali yatangaza dharura ugonjwa wa Polio
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 19, 2023