Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax ameipongeza na kuishukuru kampuni ya Mabasi ya Classic Coach, kwa uamuzi wake wa kizalendo wa kukubali kuonesha filamu ya The Royal Tour, iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kifaransa katika mabasi yake yanayofanya shughuli za kusafirisha abiria nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo -DRC.

Pongezi hizo, amezitoa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa uoneshaji wa filamu hiyo kwenye mabasi hayo, iliyofanyika jijini Kinshasa kwenye viwanja vya ubalozi wa Tanzania nchini humo Machi 17, 2023 na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo maafisa wa Ubalozi wa Tanzania na wawakilishi wa kampuni hiyo.

Baadhi ya wageni walioshiriki hafla ya uzinduzi wakiwa kwenye moja ya basi litakalotumika kuoneha filamu ya the Royal Tour.

Dkt. Tax pia amempongeza Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana na timu yake
kwa kufanikisha jambo hilo muhimu na la mfano, akiwa na mwaka mmoja tangu ateuliwe na Rais Samia kushika wadhifa huo, lakini amefanikisha mambo mengi muhimu, likiwemo la kuishawishi kampuni ya Classic yenye mabasi 50 inayotoa huduma ya usafiri wa abiria katika miji mbalimbali ya DRC, ya Kinshasa na Lubumbashi, kutangaza filamu ya the Royal Tour bila malipo.

Aidha, ameongeza kuwa mabasi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Mtanzania, Amir Abdallah anayeishi Lubumbashi, hayatumiwi na Wakongo pekee bali yanatumiwa pia na raia wa nchi nyingine, hivyo ni fursa nzuri ya kuitangaza Tanzania na fursa za uwekezaji, biashara pamoja na utalii ili kutimiza azma ya ilani ya CCM ya kuvutia watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax akitoa maelezo mafupi kwa wageni (hawapo pchani) walioshiriki hafla ya uzinduzi wa kuonesha filamu ya the Royal Tour katika mabasi ya kampuni ya Classic Coach. Wengine katika picha, watatu kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana na watatu kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

Waziri Tax pia ametoa wito kwa makampuni mengine na sekta binafsi, zijitokeze kushirikiana na Serikali katika jitihada za kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Tax amesema hafla hiyo ya uzinduzi ni sehemu ya kusherehekea miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan tokea aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Machi 2021, ambapo mafanikio mengi yamepatikana ndani ya kipindi hicho cha uongozi wake.

Athari kimbunga Freddy, JWTZ kusafirisha msaada Malawi
Chuo Ustawi wa jamii chawafunda Wadada wa kazi majumbani