Wakati mazungumzo ya Serikali nyingi Duniani yakihusisha mabadiliko ya hali ya hewa, pia kumekuwa na msisitizo wa mapambano ya kuhama kutoka njia za awali na kwenda katika matumizi ya nishati safi kama sehemu ya utekelezaji na kuheshimu ahadi zilizotolewa katika Mkataba wa Paris na ahadi za fedha za kukabiliana na janga hilo bila kuhusisha haki za binadamu.
Hii inatokana na ukwei kuwa, mara kwa mara katika maongezi na mijadala ya walio wengi kinachokosekana ni utambuzi wa kutosha kwamba shida ya hali ya hewa inaathiri sana ubinadamu ikikumbukwa kuwa mwaka huu wa 2022 tuliendelea kuona hali mbaya ya hewa ikiharibu maisha ya watu, nyumba, jamii na afya.
Kwa mfano, nchini Pakistani, uharibifu wa mafuriko ulikuwa mkubwa, na kuwaacha karibu robo tatu ya watu milioni bila kuwa makazi salama na ya kutosha, na kuua karibu watu 1,700, huku Malaysia pia ikikumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababisha zaidi ya watu 8,000 kuyahama makazi yao na kusababisha vifo vya watu 50.
Hali hii, pia ilileta kitu kinaitwa ‘Tropical Cycle Gombe’ ambayo iliua zaidi ya watu 50 nchini Msumbiji na huko Ufilipino, Dhoruba ya Tropiki Megi iliua zaidi ya watu 120, huku pale Afrika Kusini watu wasiopungua 435 wakifariki wakati wa mafuriko ya KwaZulu-Natal, na nyumba 8 584 zikiharibiwa.
Vilevile, hali ya hewa pia ikaipiga Eastern Cape, ukame unaoanza polepole katika Ghuba ya Nelson Mandela ukaendelea kutishia upatikanaji wa maji salama, ya kutosha na ya kutegemewa kwa maelfu ya wakazi hali ambayo pia imeikumba Kenya kiasi cha kuleta mvutano baina ya viongozi wa Taifa hilo juu ya uagizwaji wa nafaka kutoka Ulaya.
Matukio haya yote, ambayo nimeyaorodhesha kwa uchache yanaathiri haki za binadamu za huduma za msingi, lakini jambo hili halijajumuishwa kikamilifu katika mikataba ya hali ya hewa, sheria za hali ya hewa au mijadala ya hali ya hewa na ilirudiwa wakati muswada mpya wa Mabadiliko ya Tabianchi uliowasilishwa ukiwa hauna mbadala unaozingatia haki za binadamu.
Ingawa haya yote yametukia bila kuleta madhara makubwa katika nchi yetu, bila shaka Serikali ni lazima izingatie wito wa mashirika ya kiraia ya kutumia muswada huo kuelezea majukumu ambayo yanalinda haki za binadamu za vizazi vya sasa na vijavyo dhidi ya athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa ili kuondoa imani haba ya jamii juu ya madhara yanayoweza kujitokeza.
Nasema hivi kwa sababu, ukiwasikiliza wakazi wengi walioathiriwa na mafuriko, ukame na hata ukosefu wa maji, wao wanaelezea wazi kuwa changamoto zinazoingiliana, za maendeleo endelevu, mabadiliko ya hali ya hewa na ukosefu wa usawa unaohitaji njia mpya ya watawala kuja na majibu yatakayokuwa na tija.
Wanasema, lazima kuwe na kipaumbele cha ulinzi wa haki za binadamu kama ilivyoainishwa katika katiba, yaani hatua za uwajibikaji lazima ziimarishwe ili kukabiliana na changamoto za kimuundo na kukosekana kwa usawa wa kimfumo ili kujenga ustahimilivu wa watu wanaokabiliwa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.
COP27, mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, wanaitaja kama fursa ya kuonesha ulimwengu kwamba serikali ya Tanzania ipo imara na inaendelea kujitolea kukabiliana na dharura ya hali ya hewa na majanga mengine kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia, na uwepo wa matumaini ya maamuzi ya viongozi wa dunia pale Sharm el-Sheikh, Misri, kama matokeo ya kudumu kwa wanadamu wote.
Wakati ni sasa wa kuchukua hatua za haraka na za ujasiri juu ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaweka watu na haki za binadamu katikati yake na Mataifa pamoja na mambo mengine ni lazima yapambanie haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki za kazi kutokana na jamii kuathiriwa zaidi na mgogoro wa hali ya hewa.
Serikali pia inatakiwa kuchukua hatua za haraka ili kuyafanyia kazi malengo ya utoaji wa hewa chafu ya 2030 ambayo yanawiana na hitaji la kuweka ongezeko la wastani wa joto duniani chini ya 1.5°C yakiakisi ulazima na dhima ya kihistoria ya maeneo athiriwa ya hali ya hewa na pia uchumi wa eneo husika.
Kingine ni kuanzisha kituo cha kufadhili na kushughulikia hasara na uharibifu, ikiwemo kuunda mpango kazi kwa kushirikiana na nchi wahisani, ili kuongeza michango ya kufadhili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuunda mpango kazi madhubuti na unaolingana na haki za binadamu wa utekelezaji wa uwezeshwaji.
Ikumbukwe kuwa, si kwamba Serikali yetu haiwajibiki la hasha, tumeshuhudia mapambano mengi katika nyanja mbalimbali yanayolenga kuliletea Taifa taswira chanya ikiwemo kwenye sekta ya elimu, afya, uchumi, biashara na hata ujenzi wa miundombinu, kongole kwa Viongozi wetu wakiongozwa na Rais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kinachosisitizwa hapa ni kuona namna gani tunaweza kuangalia madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake kwa haki za binadamu.
Hivyo, ni lazima kutambua kwamba, COP27 haikuwa ya kupeana mikono, kuchapisha habari zake mitandaoni na kupiga picha hili hapana, ila tunataraji iwe suluhisho la kuchukua hatua ambazo zitakulinda wewe, mimi, familia zetu na jamii nzima, kutokana na kuvumilia mwaka huu wa matukio ya hali mbaya ya hewa yaliyoleta athari kwa ndugu zetu maeneo mengi barani Afrika na Duniani kiujumla kwani mgogoro wa hali ya hewa ni mgogoro wa haki za binadamu.