Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema bado inaendelea kuyashikilia mabasi 70 ya kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), ambayo hadi sasa ni zaidi ya miezi 13 tangu yakwame katika Bandari ya Dar es Salaam.
Februari 13, mwaka jana Udart ilitangaza kupokea mabasi hayo makubwa 70 yenye thamani ya Dola za Marekani 270,000 kutoka China, lakini yameshindwa kulipiwa kodi ili kuyakomboa bandarini.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, aliliambia Nipashe juzi kuwa mamlaka inaendelea kuyashikilia mabasi hayo na upigaji mnada utatokana na uamuzi wa kisheria na kiutawala wa kodi.
“Bado hayajalipiwa na tunaendelea kuyashikilia ila kiasi gani cha kodi ambacho tunadai ni mawasiliano kati yetu na mteja tu,” alisema.
Kayombo alipoulizwa ukomo wa kuyashikilia na suala la kuyapiga mnada alisema, “Hayo ni maamuzi ya kisheria na kiutawala wa kodi,” alisema.
Februari 16, mwaka jana Udart ilitangaza kupokea mabasi makubwa 70 yenye thamani ya Dola za Marekani 270,000 kutoka China ambayo yangeongeza nguvu ya kupunguza msongamano wa abiria vituoni.
Mabasi hayo yalipokelewa siku hiyo Bandari ya Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Charles Newe, ambaye alisema kuwa mabasi hayo ni yale yenye urefu wa mita 18 ambayo yameunganishwa katikati hivyo kufanya idadi yake kwa wakati huo kufikia 109