Waziri wa kilimo Japhet Hasunga amemwagiza mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti, kusimamia chama kikuu cha ushirika mkoani Kagera -KCU 1990 LTD na chama kikuu cha ushirika katika wilaya za Karagwe na Kyerwa -KDCU kulipa kiasi cha fedha shilingi billioni 20 kwa wakulima wa kahawa ndani ya siku tatu.
akiwa mjini Bukoba katika ziara ya utekelezaji wa kazi ya wizara yake, amesema malipo ya wakulima yamecheleweshwa kutokana na kahawa kukosa kupelekwa sokoni baada ya baadhi ya nchi kufunga mipaka kutokana ugonjwa wa homa kali ya mapafu – COVID 19.
Waziri Hasunga amesema kuwa ili kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao, serikali imelazimika kuongeza mkopo kutoka benki ya kilimo na kuwa hivi sasa fedha zote wanazodai wakulima zimepatikana.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameshukuru kwa hatua hiyo na kutumia fursa hiyo kuwaomba wakulima kuandaa na kuhifadhi kahawa yao katika mazingira bora, ili ziweze kupata soko.