Serikali kupitia Wizara ya Afya, imesema inakamilisha mapitio ya miundo ya kada za afya yanayotazamiwa kukamilikai Mei, 2023 ambapo yatawasilishwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala na Bora kwa ajili ya kupata idhini.
Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum, Dkt. Alice Kaijage katika mkutano wa kumi na moja kikao cha 15 Bungeni jijini Dodoma huku akiongeza kuwa mara baada ya kupata idhini watumishi wa afya wataanza kunufaika na maboresho hayo.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel.
Amesema, “Wizara inakamilisha Mapitio ya Miundo ya kada za afya, kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2023 na kuwasilishwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala na Bora kwa ajili ya kupata idhini.”
Aidha, Dkt. Mollel ameongeza kuwa, kukamilika kwa maboresho hayo pia kutasaidia kukidhi mahitaji ya kiutumishi kwa wataalamu mbalimbali wa afya, wakiwemo Madaktari Bingwa na Wataalamu waliopata fursa ya kujiendeleza.