Timu ya madaktari imewasili katika eneo la Kargi lililopo jimbo la Marsabit kaskazini mwa nchi ya Kenya, kuchunguza taarifa za vifo vya watu tisa vinavyodaiwa kusababishwa na ugonjwa usiojulikana.
Watu hao, walifariki katika kipindi cha wiki mbili zilizopita wakati watu wengine themanini wakiendelea kupokea matibabu kwenye eneo hilo, baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa tata.
Wakaazi wa eneo hilo wanadai kuwa, mlipuko wa ugonjwa huo umeendelea kuwa kitisho huku Mwakilishi wa wadi ya Kargi, Christopher Ogom akiilaumu idara ya afya kwa kutowajibika licha ya ripoti kutolewa muda mrefu.
Hata hivyo, idara ya afya ya Marsabit imethibitisha kuwapeleka maafisa wa afya katika eneo hilo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ugonjwa huo, ambapo awali Msemaji wa kaunti ya Marsabit, Barille Abduba alikana ripoti za mlipuko wa ugonjwa huo, akisema yalikuwa magonjwa ya kawaida.