Madaktari nchini Uganda wamempigia magoti Rais wao Yoweri Museveni wakimuomba kuongeza muhula mwingine wa kuwa Rais wa Taifa hilo wakisema ameboresha na kubadilisha sekta ya afya ikiwemo ustawi wa wafanyakazi wanaotoa huduma za matibabu.
Tukio hilo la Desemba 3, 2022, limetokea katika Viwanja vya Uhuru Kololo jijini Kampala, wakati wa kongamano la Vijana na Uwekezaji ambapo Rais Museveni alikuwa mgeni rasmi ambapo Rais wa Chama Cha madaktari Uganda Dkt. Odingo alimsifia Rais Museveni Kwa kuboresha huduma za afya nchini humo.
Amesema, “Umeboresha Hospitali za rufaa za mikoa, Hospitali kuu zinapandishwa hadhi hadi kufikia kiwango cha Hospitali za rufaa za mikoa, Watu wetu wanaweza kupokea huduma katika maeneo yao mahususi.”
Dkt. Odingo ameongeza kuwa, “Mheshimiwa, Yoweri Kaguta Museveni, umekuwa injini ya kuboresha ustawi wa wafanyakazi wa afya na hivi sasa mhudumu wa afya anayelipwa mshahara mdogo anapata Shilingi 1.4 milioni kutoka UGX 600,000.”
Hata hivyo, kumekuwa na maoni tofauti juu ya tukio hilo ambapo Luboyera Charles Grace, amesema kitendo kilichofanywa na Madaktari hao mbali na kuwa ni cha kushangaza pia ni usaliti na urahisi wa kushusha heshima ya taaluma yao.
Kwa upande mwingine, baadhi ya watu hawakushtushwa na kitendo hicho wakidai Madaktari hao wametimiza wajibu wao na tayari wamefikisha ujumbe kwa Rais.