Madereva Bodaboda wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi wamekula kiapo cha uaminifu cha kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vya ngono na mimba za utotoni zinazo sababisha kukatisha haki yao ya kuendelezwa.
Kiapo hicho kimeongoza na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa “Kampeni ya Mimi ni Msichana Najitambua Elimu Ndio Mpango mzima” iliyozinduliwa tarehe 11 Oktoba, 2017 kwa lengo la kuhamasisha wananchi kupambana na kuzuia matukio ya mimba za utotoni katika jamii zetu.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa ili kufanikisha kutokomeza mimba za utotoni hatuna budi kuweka ushirikiano baina ya wazazi, walezi, jamii, Serikali na wadau wengine ili kuwaepusha watoto wa kike kupata vishawishi vya mahusiano ya kingono katika umri mdogo na hatimaye kupata mimba za utotoni.
Ameongeza kuwa lengo la Kampeni ya “Mimi ni Msichana Najitambua Elimu ndio Mpango Mzima” imelenga kuunganisha nguvu za pamoja za wanajamii wakiwemo madreva wa Bodaboda kushirikiana na Serikali kuzuia na kutokomeza matukio ya mimba za utotoni katika ngazi ya jamii na shuleni.
“Niseme kampeni hii itasaidia kwa asilimia kubwa kuunganisha nguvu zetu kama wananchi na sisi Serikali katika kutokomeza vitendo hivi viovu” amesisitiza Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amewaasa madereva hao kuondokana na tamaa za kujihususha na mahusiano na kingono na watoto wadogo bali wao kuwa walinzi wao katika kutokomeza suala mimba kwa watoto wetu.
Amewataka kufichua vitendo vyovyote vyenye ushawishi wa mahusiano yanayosababisha mimba kwa watoto wa kike ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kuweka mikakati ya kupambana na wanaume na vijana wakware wanaotumia fursa zao kuwa na mahusiano maovu na watoto wa kike katika Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi ambao ndio unaoongoza kitaifa kwa kuwa na asilimia 45.
Mmoja wa dereva Boda boda wa Wilaya ya Mpanda Bw. Juma Salum kwa wakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kuandaa Kampeni hiyo itakayowajengea uelewa wananchi kusaidiana katika kuwalinda watoto wa kike kwa kuweka miundo mbinu salama ya kusomea na kujifunzia ili kupunguza kiwango cha mimba za utotoni kwa silimia 50 ifikapo mwak 2021/22.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alikuwa na ziara ya siku mbili mkoani Katavi kuhamasisha wananchi kupambana na kuzuia mimba za utotoni kupitia “Kampeni ya Mimi ni Msichana Najitambua Elimu Ndio Mpango mzima”.