Polisi Mkoa wa Arusha imefanya ukaguzi wa magari ya shule zaidi ya 150 na kutoa elimu kwa wamiliki wa shule na madereva wa magari hayo, toka maeneo mbalimbali jijini humo.
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi, SP Solomon Mwangamilo amesema zoezi hilo ni endelevu na si la hiyari, na kwamba hawatasita kuchukua hatua kwa mmiliki atakaye kaidi kuhudhuria zoezi hilo lililoanza kufanyika Septemba 5, 2022.
Amesema, “Sote tumeshuhudia namna vijana na Watoto wetu wanavyopoteza maisha katika ajali za magari haya ya shule, ambapo amesema ukaguzi huu na elimu kwa wamiliki na madereva utasaidia kupunguza ajali ambazo zimekatisha ndoto za vijana wetu ambao ni hazina kwa taifa.”
Kwa upande wao, baadhi ya wamiliki wa shule waliojitokeza katika zoezi hilo, wamelishukuru Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani, kuweka utaratibu wa ukaguzi wa magari ya shule wa mara kwa mara utakaosaidia kuongeza umakini na kuepusha ajali.