Maelfu ya wafuasi wa upinzani wameandama mjini Minsk wakishinikiza kuondoka kwa utawala wa kiongozi wa kiimla wa Belarus Alexander Lukashenko.
Licha ya kuweko ulinzi mkali na waandamanaji kadhaa kutiwa nguvuni , bado kumeendelea kuwako kwa shinikizo la kumtaka Lukashenko kuondoka madarakani.
Maandamano ya Belarus yameingia wiki ya tatu tangu kufanyika uchaguzi wa rais wa Agosti 9 ambao Lukashenko alijitangaza mshindi , Kiongozi wa upinzani Svetlana Thikanovskaya anasema yeye ndiye aliyekuwa mshindi wa kweli.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 100,000 wamehudhuria maandamano ya jana ambao yameelezwa kuwa makubwa kuwahi kushudiwa nchini humo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa uliokuwa muungano wa Kisovieti.
Umati ulikusanyika nje ya makaazi rasmi ya rais huyo, Kasri la Uhuru, ambalo lililindwa na polisi wa kuzima ghasia na vikosi maalum vikisaidiwa na walenga shabaha waliokuwa kwenye mapaa.