Maelfu ya wananchi wa Zimbabwe jana waliandamana kumuunga mkono Rais Emmerson Mnangagwa kupinga vikwazo vilivyowekwa na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya dhidi ya nchi hiyo.
Marekani na Ulaya imewawekea vikwazo maafisa wengi waandamizi wa Zimbabwe pamoja na Rais Mnangagwa kwa madai ya kukiuka haki za binadamu na udanganyifu katika uchaguzi mkuu, miaka iliyopita.
Maandamano hayo ya Ijumaa yaliratibiwa na Serikali na ilitangazwa kuwa ni siku ya mapumziko. Raia wengi nchini humo waliitikia wakiandamana kuelekea kwenye uwanja wa mpira.
Rais Mnangagwa alihutubia katika uwanja huo akieleza kuwa vikwazo hivyo vimeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa Zimbabwe.
Waandamanaji wakiwa kwenye fulana zenye jumbe mbalimbali na mabango ya kupinga vikwazo hivyo, walizielezea Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa ni ‘waovu’ na watengeneza silaha nzito za kuangamiza binadamu.
Mwaka 2001, Marekani iliweka vikwazo vya kiuchumi kwa viongozi 85 wa Zimbabwe akiwemo Robert Mugabe aliyekuwa Rais wakati huo na Mnangagwa; pamoja na viongozi wengine wa chama tawala cha ZANU-PF. Walieleza kuwa chanzo cha vikwazo hivyo ni kutowatendea haki wapinzani wa Serikali pamoja na udanganyifu kwenye chaguzi.
Jana, Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi ilitangaza kuiunga mkono Zimbabwe ikizitaka nchi za Ulaya na Marekani kuiondolea vikwazo kwani vinawaathiri wananchi.