Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi -OSHA, umeyachukulia hatua maeneo ya kazi 1,588 ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya kwa kuyapa hati ya maboresho, na kuyatoza faini maeneo mengine 105.
Hayo yamebainishwa hii leo Machi 4,2023 Jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda na kuongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya usimamizi wa Sheria ya Usalama na Afya, yenye lengo la kuzuia ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi,
Amesema, pia OSHA imefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi kufukia 11,953 sawa na asimilia 276 huku ongezeko la Wafanyakazi waliopata mafunzo ya afya na usalama mhala pa kazi yakifikia asilimia 175, na kuongeza kuwa idadi ya kaguzi zilizofanyika nazo zimeongezeka kutoka 104,203 hadi kufikia 322,241 sawa na asilimia 132.
“Lipo ongezeko la asilimia 175 ya wafanyakazi waliopata mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia wafanyakazi 43,318, na ni jumuishi ya uundwaji wa kamati za Usalama na Afya, mafunzo ya kufanya kazi za mazingira ya juu, mafunzo ya huduma ya kwanza,” amesema Mwenda.
Aidha, amefafanua kuwa ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi limefikia asilimia 320 kutoka watu 363,820 hadi kufikia watu 1,112,237 waliopimwa katika kipindi tajwa, likitokana na kupunguzwa kwa ada mbalimbali na kuboresha mifumo ya usimamizi ambayo imewezesha maeneo mengi ya kazi.