Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini nchini wakiwemo wa Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqaama kuongeza juhudi katika kutoa mafunzo ya dini ili kupunguza na kisha kuondoa kasi ya mmomonyoko wa maadili.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Novemba 5, 2022 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya Istiqaama Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam, na kusema jamii imekuwa ikishuhudia vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili.
Amesema, viongozi wa dini na wale wa umma wana wajibu wa kuilea jamii kwa kutoa mafundisho sahihi na endelevu ya dini, ili wawezesha kutambua na kufuata yote yaliyo mema kama ilivyo amrishwa na Mwenyezi Mungu.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Jumuiya ya Istiqaama na Jumuiya nyingine mbalimbali za dini ambazo zimejikita katika kutoa mafunzo ya kiroho yanayoifanya jamii kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuwawezesha wananchi kuishi kwa amani,” amesema Waziri Mkuu.
Awali, akizungumza kwa niaba ya waumini Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqamaa, Sheikh Seif Ally Seif, aliishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa taasisi za dini na alimpongeza Rais Mheshimiwa Samia kwa kusimamia haki upendo na kujenga umoja wa kitaifa, hivyo kuifanya nchi kuendelea kuwa katika uelekeo mzuri.
Alisema, lengo la jumuiya ya Istiqaama ni kutoa mafundisho ya kidini na kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama elimu ambapo wana shule 14 Tanzania Bara na Zanzibar, pia wanatoa huduma za afya pamoja na uchimbaji wa visima vya maji.