Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amefika Wilayani Hanang, Mkoani Manyara kwa lengo la kutoa pole na kukabidhi mchango wa wadau na Wizara kwa Wananchi walioathirika na mafuriko wilayani humo.

Wakati akitoa salamu hizo za pole hii leo Desemba 11, 2023, Ulega alisema Wizara imepokea kwa masikitiko makubwa tukio la mafuriko hayo yaliyotokea na kusababisha kupotea kwa maisha ya watanzania pamoja na uharibifu wa mali na mifugo.

Amesema, kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya mifugo na uvuvi wakiwemo ASAS, Bajuta International, Dalberg International, Karie Kinana, APOKA, TAFMA, TABROFA na TPBA) kwa pamoja wameandaa vitu mbalimbali na kuvikabidhi kwa Kamati ya Maafa ya Kitaifa kwa ajili ya uratibu wa namna nzuri ya kuvifikisha kwa familia na walengwa wote.

Miongoni mwa vitu vilivyokabidhiwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama kwa niaba ya waathirika wa mafuriko hayo ni pamoja na Ng’ombe 13, Mbuzi 20, Trei 90 za mayai, Fedha tasilimu jumla ya shilingi Milioni 5, Maziwa katoni 300, Sembe, Maharage na Chumvi.

Aidha, alibainisha kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Kamati ya Taifa ya Maafa na Uongozi wa Mkoa na Wilaya ili kubaini uharibifu wote wa miundombinu ya mifugo na kuirejesha katika hali yake kwa haraka ili kuhakikisha mifugo inaendelea kupata huduma stahiki na kuwezesha wafugaji kunufaika na mifugo yao kwa maendeleo ya nchi.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga alitoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wadau mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.

Kalvin Phillips anasakwa Old Trafford
Juma Mgunda atuliza presha Simba SC