Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameainisha changamoto zinazopaswa kupewa kipaumbele ikiwemo kufungamanisha ukuaji wa uchumi na sekta za uzalishaji.

Rais Samia amesema hayo kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru na Mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Aidha, ametaka sekta mbalimbali za uzalishaji ziimarishwe zaidi ikiwemo Kilimo ambayo inakua kwa asilimia 4 tu kwa sasa tofauti na inavyotakiwa huku akisisitiza kuimarishwa kwa ushiriki wa sekta binafsi ndani na nje ya nchi ili kufanya wenyeji kuwa na utayari wa kupokea na kushirikiana na wageni wanaokuja
kuwekeza na kufanya biashara nchini.

Rais Samia amesema dira hiyo mpya itatakiwa kuzingatia kigezo cha kuongeza pato la kila mwananchi kufikia dola za Kimarekani 3,000 kwa mwaka ambacho hakikufikiwa katika dira ya mwaka 2000-2025.

Amesema kushindwa huko kulisababishwa na ukuaji wa uchumi kutojielekeza kwenye sekta zinazogusa maisha ya watu wengi, hivyo umasikini vijijini
haujapungua kwa kasi iliyotarajiwa.

Kuhusu suala la Maadili ya Taifa (ethos), Rais Samia amesema ni muhimu taifa kuwa na watu mahiri, makini na waadilifu ili kupata jamii inayochukia rushwa kila mahali, inayojituma na kufanya kazi bila kusukumwa na inayopinga na kulaani ukwepaji kodi.

Hata hivyo, ametoa wito kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi (Diaspora), kushiriki kutoa maoni katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo kupitia njia za kisasa zitakazoainishwa na Tume ya Mipango.

Miaka 62 ya Uhuru: Wafungwa wapata msamaha
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 10, 2023