Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetoa wataalamu watano wa masuala ya Saikolojia ambao wataungana na wataalamu wengine ambao wanaendelea kutoa huduma katika kambi tatu za waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope na mawe Hanang mkoani Manyara yaliyotokea Disemba 3, 2023
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mkuu wa Kitengo cha Ushauri na Unasihi wa Chuo hicho, Dkt. Bernadetha Rushahu amesema wameleta wataalam hao ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi waliopata maafa hayo kwa kuzingatia madhara waliyopata ikiwemo ya kisaikolojia na kimwili, hivyo ni vizuri kuwasaidia katika maeneo yote ili warejee katika hali zao.
“Tumetoa wataalamu hawa lengo ni kuongeza nguvu ili kuwafikia waathirika wote kwa kuhakikisha tunawapa ushauri utakaowafaa kuondokana na hofu na msongo wa mawazo, watayafikia makundi yote ikiwemo watoto, wazee na watu wenye ulemavu na kuhakikisha kuwa hawaachi kundi lolote bila kuwahudumia,” alisema Dkt. Benrnadetha.
Akiwapokea wataalam hao, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, ameshukuru Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa utayari wao kwa kujitolea wataalam hao na kusema watawafaa maana wanahitaji huduma zote muhimu hata za kiroho ili waendelee kuimarika.
Amesema, “Mmefanya vizuri sana Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kupokea misaada mbalimbali na kwa kushirikiana na Mkoa hivyo hii ni sehemu ya msaada wenu kwetu, Serikali inaendelea kutoa wito kwa wadau kujitokeza na kuchangia kuendelea kusaidia ndugu zetu hawa,asanteni sana.”