Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limeanza hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi wa utafutaji wa mafuta katika bonde la mto Manonga, baada ya utafiti kubaini uwepo wa miamba yenye viashiria vya mafuta katika bonde la mto huo.
Akitambulisha mradi huo kwa uongozi wa mkoa wa Shinyanga, mtaalam mshauri wa mradi Dkt. Allan Mzengi, kutoka TPDC amesema mradi huo unaanza na hatua ya awali ya kuangalia athari za kimazingira, wilaya Kishapu mkoani Shinyanga hatua itakayoshirikisha wadau kuanzia ngazi ya mkoa hadi Kata.
Dkt. Mzengi, amesema licha ya kuangazia suala la kimazingira, hatua ya pili ya mradi huo itakuwa ni ujenzi wa mkuza katika eneo ambalo mradi utatekelezwa na baadaye kuweka vilipuzi vitakavyosaidia kubaini maeneo ya ujenzi wa visima vya majaribio ya utafutaji mafuta katika eneo la mradi.
Kwa upande wake mjiolojia kutoka TPDC Gaston Canuty, amesema tayari TPDC imeishachimba visima vifupi katika eneo la mradi ili kubaini miamba yenye uwezekano wa kuhifadhi mafuta ambapo amesema mradi unakusudia kwenda mbali zaidi, kuangalia mafuta yako wapi chini ya ardhi.
Mradi huo ujulikanao kama Eyasi-Wembele unatatekelezwa katika Mikoa ambayo mto huo unapitia ikiwemo bonde la Ziwa Eyasi na bonde la mto Manonga unaopatikana katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida na Manyara.