Wizara ya Nishati, Taasisi za Serikali Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA, ni kati ya Taasisi zilizopewa kongole na Umoja wa Wamiliki wa Vituo Vya Mafuta Tanzania – TAPSOA kwa kuweka utaratibu mzuri wa kupakia mafuta kwa masaa ya ziada, ili kuhakikisha kasi ya usambazaji wa mafuta nchini inaendelea.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAPSOA, imeeleza kuwa kutokana na foleni kubwa katika upakiaji wa mafuta katika maghala mbalimbali nchini wameamua kufanya kila jitihada kuhakikisha vituo vya mafuta vinapata nishati hiyo bila kuchelewa kwani utaratibu uliowekwa utasaidia kupunguza msururu wa magari yaliyojazana kwenye maghala ya mafuta maeneo mbalimbali nchini.
Wamesema, “kwa kiwango kikubwa, magari mengi yamekua yanapakia mafuta usiku na mchana, ili kuepusha taharuki ya kukosa mafuta. Pia TAPSOA wanawashukuru wenye maghala ya mafuta yaani OMC’s ambao wamekuwa na ushirikiano wa karibu katika kumaliza hizi changamoto kwa wakati na kwa haraka.
Hata hivyo, TAPSOA wamesema wanaendelea kuwasihi wanachama wake na wateja kuwa watulivu kwani jitihada zinaendelea na magari yanapakia mafuta katika maghala mbalimbali, ingawa huenda kukawa na ucheleweshwaji kutokana na hali ya kijiografia ya nchi ilivyo na magari yapo njiani kupeleka mafuta vituoni na hakuna eneo litakalokaukiwa na mafuta.