Kundi la kigaidi linalojiita ‘Islamic State of Iraq and Syria’ (ISIS) kwa mara ya kwanza limetajwa kufanya mashambulizi ya mlengo wa kigaidi Jerusalem nchini Israel.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kuwa shambulizi la kutumia roli lililowaua watu wanne na kujeruhi wengine 17 lilifanywa na kijana wa Palestina aliyetumwa na kundi la ISIS.
Israel ilifanya kikao cha dharura cha kabineti ya usalama ambacho ingawa hakikutoa vielelezo kuhusu mtu huyo, kilimtaja kuwa mfuasi wa ISIS.
“Tunajua kumekuwa na mlolongo wa mashambulizi ya kigaidi. Kuna uhakika kuwa kunaweza kuwa na muungano kati yao [ISIS], kutoka Ufaransa hadi Berlin, na sasa Jerusalem,” alisema Netanyahu.
Mshambuliaji huyo aliyetambulika kwa jina la Fadi Qunbar mwenye umri wa miaka 28, raia wa Palestina alitumia lori kubwa kuwagonga watu hao lakini alipigwa risasi na kuuawa papohapo baada ya kutekeleza tukio hilo.
Watu kadhaa wamekamatwa kutokana na tukio hilo wakiwemo majirani zake na wana familia wake watano.