Kiungo wa klabu ya Arsenal Mesut Ozil amesema yupo tayari kusaini mkataba mpya na klabu hiyo, lakini itategemea na mipango ya bosi wake Arsene Wenger.

Mustakabali wa kiungo huyo kutoka nchini Ujerumani umekua katika hali ya sintofahamu klabuni hapo, kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita sambamba na mshambuliaji Alexis Sanchez, ambapo wote kwa pamoja wanatakiwa kusainishwa mikataba mipya.

Ozil amefunguka kuhusu mpango wa kusaini mkataba mpya na uongozi wa Arsenal, alipohojiwa na jarida la michezo la nchini kwao liitwalo German magazine Kicker, ambapo amesema yupo tayari kufanya hivyo na wala asifikiriwe vibaya na mashabiki wa The Gunners.

Amesema kila jambo klabuni hapo linapangwa na Arsene Wenger, na anaamini meneja huyo ambaye alimsajili akitokea Real Madrid miaka minne iliyopita, atakua katika harakati za mwisho za kumaliza mikakati aliyoweka kwa ajili ya kuhakikisha anabaki Emirates Stadium.

“Kwa kweli nina furaha ya kuendelea kuwa hapa, ninataka klabu na mashabiki kwa ujumla walifahamu hilo, sina tatizo la suala la kusaini mkataba mpya.”

“Klabu inafahamu nipo hapa kwa ajili ya maelewano mazuri yalijengeka baina yangu na Arsène Wenger. Alinisajili na ananiamini kwa kazi ninayoifanya, hivyo kila hatua ya maandalizi ya mkataba mpya ipo mikononi mwake.” Alisema Ozil.

Kufunguka kwa Ozil, kumekuja baada ya gwiji wa Arsenal Thierry Henry kutangaza hadharani kuhusu mustakabali wa kiungo huyo pamoja na Alexis Sanchez ambao wamekua na hali ya kutokueleweka kuhusu hatua ya kusaini mikataba mipya.

Henry alisema ni wakati mzuri kwa wawili hao kuonyesha wazi kuhusu suala hilo, na wanapaswa kufanya hivyo kwa kuwaridhisha mashabiki, ambao wameonyesha kuwahusudu kwa kipindi chote tangu waliposajiliwa klabuni hapo.

Ozil aliongeza kuwa, anaheshimu kauli iliyotolewa na Henry, na katu hawezi kuipinga kutokana na kufahamu umuhimu wake klabuni hapo.

“Kila mmoja ana haki ya kusema kuhusu suala hili, na siwezi kumpinga, lakini bado ninasisitiza kuwa mustakabali wangu ndani ya Arsenal utaendelea kuwa mikononi mwa Arsene Wenger.”

Rais wa zamani wa Iran afariki dunia
Magaidi wa ISIS waishambulia Israel, Netanyahu anena