Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limefanikiwa kuyakamata magari 25 kwa kukiuka amri ya IGP kwa kuyafunga magari yao ving’ora na taa kali pamoja na gari jingine jipya aina ya Probox kukutwa likitumia namba ambazo zipo kwenye gari lingine.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Giles Muroto amesema kuwa magari hayo yamekiuka amri ya IGP iliyoagiza kutokufunga ving’ora na taa kali kwa gari za kawaida bila utaratibu huku gari hilo jipya lilikamatwa likiwa na namba ya gari lingine linalopatikana Wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi mkoani humo limekamata zaidi ya mita elfu tatu za nyaya zinazomilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, gari linalosadikika halikupatikana kihalali na masanduku mawili yaliyokuwa na bangi ikisafirishwa Jijini Tanga.
Akizungumzia kukamatwa kwa nyaya za umeme, Mhandisi Miradi ya REA awamu ya tatu mkoani Dodoma, Tumaini Chonya amesema kupatikana kwa nyaya hizo ni hujuma zinazofanywa na baadhi ya watu wachache.