Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, umesisitiza kikosi chao kuendelea kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, licha ya baadhi ya wadau wa soka kukitazama tofauti baada ya kuanza kwa kasi ndogo.
Simba SC ilianza msimu mkoani Mara katika mji wa Musoma dhidi ya Biashara United na kuambulia sare ya 0-0, kisha ikacheza dhidi ya Dodoma Jiji FC mjini Dodoma na kuambulia ushindi wake wa kwanza wa bao 1-0.
Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Simba SC, Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo Crescentius Magori, amesema bado malengo ya timu hiyo msimu huu kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, yapo palepale.
“Malengo yetu ni kuhakikisha kuwa tunautetea ubingwa wa ligi kuu msimu huu, tunafahamu kuwa sio rahisi kwa kuwa kuna timu nyingi ambazo zina malengo kama yetu na tumejiandaa kupambana nazo.”
“Haikuwa rahisi kutwaa ubingwa katika misimu minne mfulululizo, tulipambana haswa kuyafikia mafanikio yale, hivyo hatutokata tamaa.”
“Tutasimama kwa pamoja kuhakikisha mafanikio ya Simba yanaendelea kuwepo, hivyo msimu huu ubingwa hauendi popote, unabaki kwetu.”
Msimu huu 2021/22, Simba SC inawania taji la tano mfululizo la Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufanikiwa kutwaa taji hilo kwa misimu minne mfululizo.