Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) na mwenzake mmoja,mtaalamu wa Tehama, Theodory Giyani (36), wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Magoti na Giyani, wanakabiliwa na mashtaka ya kushiriki genge la uhalifu, kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa kwa lengo la kutenda uhalifu na utakatishaji fedha kiasi cha Sh17milioni.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega na jopo la mawakili wanne wa Serikali ya Tanzania.
Kabla ya kusomewa mashtaka hao, hakimu Mtega amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP).
Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai Magoti na Giyani, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 137/2019.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2020 itakapotajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Magoti alikamatwa Ijumaa asubuhi jijini Dar es Salaam na watu ambao walikuwa wamevaa kiraia na kuzuka taharuki kuwa ametekwa na watu wasiojulikana.
Baadaye jioni ya siku hiyo hiyo Kamanda wa polisi wa Dar es Salaam Lazaro Mambosasa akathibitisha kuwa mwanaharakati huyo pamoja na wenzake watatu hawakutekwa na badala yake wamekamatwa kwa tuhuma za jinai ambazo hakuzitaja.