Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Balozi Ali Davutaglu katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kabudi amemweleza Balozi Davutaglu kuwa Uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki ni wa muda mrefu na mahusiano hayo ni imara hadi sasa.

“Ushirikiano wa Tanzania na Uturuki ni wa muda mrefu na ni imara kwa kweli, pamoja na mambo mengine uhusiano huu umekuwa ukijikita katika kuendeleza uwekezaji wa viwanda, elimu na utalii hasa katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika shirika la ndege la Uturuki,” Amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Balozi wa Uturiki nchini Tanzania, Mhe. Balozi Ali Davutaglu amesema kuwa Uturuki ni nchi ambayo imekuwa ikiheshimu taratibu za nchi ya Tanzania na ni marafiki wazuri na wa siku nyingi hivyo ataendelea kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali yanasonga mbele ili kuiwezesha Tanzania kuwa na maendeleo endelevu.

“Uwekezaji ni muhimu sana kwa nchi zetu hizi mbili na tayari nimeshawasiliana na Umoja wa Wasafirishaji na ule wa Mawakala wa Utalii Uturuki ili waweze kutembelea Tanzania pamoja na kuangalia fursa za uwekezaji kwa lengo la kuwekeza na hatimaye kukuza sekta hizi na uchumi wa mataifa haya mawili,” Amesema Balozi Davutaglu

Serikali yatoa msimamo UNHCR kuvunja makubaliano
Magoti afikishwa kizimbani kwa uhujumu Uchumi, arudi rumande