Rais Dkt. John Magufuli amechukua fomu ya kugombea Urais kwa awamu ya pili kupitia chama chake cha CCM, Fomu hiyo amekabidhiwa na Katibu Mkuu Dkt. Bashiru Ally jijini Dodoma.
Baada ya kukabidhiwa, Dkt Magufuli ameahidi kutafuta wadhamini ndani ya siku 17 ili aweze kurejesha fomu hiyo kuendana na matakwa ya kanuni za chama hicho.
”Asante sana Katibu Mkuu, naomba nianze hili zoezi la kutafuta wadhamini kwa Mwenyekiti wa CCM hapa Dodoma naye anidhamini na nitaenda mikoa yote kwasababu nimekuwa nikipigiwa simu wanataka kunidhamini hivyo naamini nitarejesha fomu yangu kwa wakati”, amesema Magufuli.
Aidha Dkt. Magufuli amesema amechukua fomu hiyo kwaajili ya kuomba nafasi ya kuipeperusha bendara ya CCM pamoja na Ilani nzuri ambayo imeandaliwa kwaajili ya miaka mitano ijayo.
Ikumbukwe kuwa Katibu mwenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole alitangaza mwisho wa kurejesha fomu za kuwania Urais ni Juni 30, 2020, na Magufuli amekuwa mwanachama wakwanza kuchukua upande wa Bara.