Rais John Magufuli ameelezwa kukerwa na kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuomba Shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kujenga ofisi wilayani Chato mkoani Geita wakati tayari wana ofisi.
“Mgema akisifiwa tembo hulitia maji,TAKUKURU msianze kutia maji…Msizungumze mambo kwa kunifurahisha mimi na kujipendekeza mtanivuruga naenda kulifungua jengo moyo ukiwa unaniuma…..” Amesema Rais Magufuli
Na kuongeza “Mmesema hapa mnataka kujenga ofisi ya TAKUKURU wilayani Chato, lakini tulishawapa jengo tena la ghorofa. Msizungumze mambo kwa kunifurahisha mimi, mjipendekeze Chato wakati nimeshaondoka kwenye Urais,”
Rais Magufuli amesema hayo katika hafla ya kuzindua majengo saba ya taasisi hiyo jijini Dodoma ambapo pia ameeleza kutoridhishwa na gharama zilizotumika kuyajenga kwa sababu ni kubwa sana.
Aidha ametoa wito kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuwatafutia TAKUKURU ofisi kwenye majengo ya serikali ili kuokoa fedha za kujenga ofisi hizo
“Natoa wito kwa viongozi wengine kushirikiana na TAKUKURU haiwezekani kiongozi Mkuu wa Mkoa au Wilaya una jengo kubwa alafu ofisi ya TAKUKURU iko kwenye nyumba ya kupanga,” Ameeleza Rais Magufuli
Ameongeza kuwa “Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe wanatafuta maeneo ambayo ofisi ya Wilaya na TAKUKURU zinakua pamoja ili tusihangaike kutenga fedha zingine za kujenga ofisi hizo”